Featured Posts

DARASA HURU: MADHARA YA KITAALAMU YA KUWA NA WENZI WENGI..

YAPO mambo mengi katika mtiririko wa maisha yetu ya kila siku yanatusumbua lakini hatujui  mahali pa kutokea. Kwa bahati mbaya mengine ni rahisi sana lakini kwa sababu ya mtindo wenyewe au namna ya mtu kuchanganua mambo, anajikuta akinyanyua mikono juu!

Mathalani, suala la uaminifu. Hapa hakuna uchawi rafiki zangu. Kuna tatizo tu la kutatuliwa. Wanawake ndiyo wahanga zaidi wa tatizo hili. Wanalalamika; wanaume zao wameporwa, wamehamia nje ya ndoa. Hawana uaminifu.
Siyo kwamba, wanawake ni waaminifu sana, la hasha! Ni suala la tabia ya mtu lakini kiukweli wanaume ndiyo wanaoongoza kwa kubaki huko nje ya ndoa zao. Wanajikuta hawapendi kukutana na wake zao nyumbani. Si hao tu, hata wale ambao ni wachumba, anajikuta ana wenzi wengine nje ya mchumba wake, mwenzake anakosa thamani kwake.
Hata kwa upande wa wanawake ni hivyohivyo, akiwa na wanaume wengi ni dhahiri kwamba, uwezo wake faragha na patna wake wa siku zote hupotea na hamu ya tendo nayo huondoka. Hebu twende pamoja tukaone zaidi kuhusu somo hili muhimu.
KWA NINI LADHA HUONDOKA?
Kama nilivyotangulia kusema katika vipengele vilivyopita, tatizo kubwa hapa ni kupoteza hamu na ladha katika ubora wake faragha. Sababu kubwa na ya kwanza kabisa inayosababisha tatizo hili ni kukutana na watu tofautitofauti.
Kubadilisha sana wenzi husababisha tatizo la ubinafsi na mwathirika hujikuta akifanya kila kitu kwa ajili yake mwenyewe.

Ukiacha hilo, huvamiwa na tatizo la sononeko kutokana na kitendo alichokifanya. Kila anapokutana na patna wake wa kudumu, moyo wake humsuta kwa usaliti alioufanya.
Hata hivyo, mazoea ya kuwa na watu tofauti kila wakati na woga wa kugundulika tabia hiyo huchangia kwa kiasi kikubwa kupoteza hamu na ladha ya tendo lenyewe.
Mbaya zaidi, kama ikitokea huko anapotoka huwa ama anasifiwa sana kuwa anajua na pengine hajui na kwa mwenzake kukawa na majibu yanayotofautiana, haraka huvamia akilini na kujikuta akipoteza hamu ya tendo.
Kuambiwa na mwenzake wa siku zote kuwa siyo mkali, halafu huko barabarani akaelezwa kuwa kazi anaiweza sana, hujikuta akishindwa kufanya kazi katika kiwango kizuri.

Tabia ya kupima au kulinganisha uwezo kutoka kwa watu tofauti husababisha mihemko kufanya kazi kwa haraka kabla ya wakati wenyewe na mwisho hamu huondoka ghafla.
KUHUSU WENZI
Kwa wenzi wanaoishi pamoja wana hatari kubwa zaidi ya kusumbuliwa na tatizo hili, maana hawana namna ya kujiondoa – tayari wapo pamoja. Mmoja akishakuwa mlowezi huko njiani, tatizo hilo likimvamia linakuwa maradufu maana kila siku anamkuta mwenzake na ni lazima awe naye.

Ni busara zaidi kwa wenzi kukaa na kujadiliana pamoja kuhusu kasoro ndogondogo zinazojitokeza faragha ili kuziba mianya ya mmoja wao kuanza kutafuta faraja nje. Kila kitu kipo ndani ya ndoa, ni suala la kujadiliana tu.
Kulea tatizo kwa muda mrefu ni chanzo cha wenzi kuanza kukimbilia nje. Kama kuna jambo la kujadiliwa, zungumzeni kwa uwazi na hiyo itawasaidia wote kwa pamoja kuwa katika uwezo mzuri wa kushiriki katika ubora wake tendo lenyewe.

TATIZO JUU YA TATIZO
Rafiki zangu, iko hivi; baada ya tatizo la usaliti kumtesa mhusika kwa muda mrefu, sasa anatengeneza tatizo jipya la kupoteza hamu ya kukutana na mwenzake. Ukishapata watu wengine ambao utaamini ni muhimu kwako, wa kwako nyumbani utamuona wa kawaida.

Utaishi naye kimazoea tu na kumwona kama ndugu yako tena wa damu. Suala la muunganiko wa kuwa mwili mmoja ni la kipekee na linapaswa kupewa nafasi yake kikamilifu. Kuchanganya mambo kunaharibu maana ya muunganiko huo lakini pia kunavuruga ubora katika tendo lililowaunganisha.
Ukishaanza kumuona mwenzako wa kawaida, hana maana na vinginevyo, kuna siku anaweza kugundua jambo hilo. Akigundua ni wazi kwamba, unamfanya aanze kufikiria kutoka nje ya ndoa/uhusiano wenu kwa lengo la ama kulipiza kisasi au kutafuta faraja anayoikosa ndani ya uhusiano wenu.
NINI CHA KUFANYA?
Kwa wale ambao tayari wana tatizo hili (wanaume kwa wanawake) jambo la kwanza kabisa kwao kufanya ni kusitisha haraka uhusiano na wenzi wengine nje ya uhusiano rasmi alionao. Kama huna ndoa na uko kwenye uhusiano (unaohusisha kukutana kimwili) na zaidi ya mpenzi mmoja unapaswa kufanya uchaguzi sahihi na kubaki na mmoja tu.

Achana na tabia ya kuangalia sinema zinazohamasisha ngono. Usipende kusoma mambo yanayohamasisha sana mapenzi. Tumia muda wako kusaka mambo muhimu kwenye mitandao maana kuna wengine hutumia fursa hiyo vibaya kwa kuangalia picha chafu, marafiki wenye lengo baya na mawasiliano yanayohamasisha uchafu.
Mpe mpenzi wako nafasi ya kwanza kwa kila kitu. Mpende kwa moyo – hili litawezekana zaidi ikiwa kweli hutakuwa na mwingine, maana rafiki zangu penzi haliwezi na halijawahi kugawanywa. Ukiwa na msimamo wa kuwa na chaguo moja, itakusaidia kurekebisha makovu ya majeraha uliyoyapata.
STAREHE NA MWENZAKO
Kama ulikuwa na tabia ya kupenda kutoka mwenyewe au na wengine ambao uliamini ndiyo wanaofaa kutoka nawe, badilisha mtazamo huo. Jenga mazoea sasa ya kutoka na mwenzako na kufurahi naye katika sehemu mbalimbali za burudani.

Fuatilia kwa makini vitu ambavyo unavipenda na pengine ndivyo vilikuwa vikikukimbiza nje, umpatie mwenzi wako. Kama ni suala la mavazi, unaweza kumshauri au kumnunulia yale ambayo yalikuwa yanakuvutia, bila shaka utasogea karibu yake taratibu na tatizo lako litatoweka moja kwa moja.
KAZI KWAKO
Kila kitu kipo ndani ya uwezo wako, ni suala la kuamua tu. Furahia penzi lako na mwenzako kwa upya sasa. Mapenzi ni sawa na uwekezaji hivyo tafuta vitu muhimu vitakavyomfanya mwenzako akuone mwenye thamani kubwa siku zote. 

GPL
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment

Note: only a member of this blog may post a comment.